User:Maziwa Makuu SMM
NAMNA YA KUTUMIA WHATSAPP KIBIASHARA Habari wote mnaotembelea mtandao huu na kusoma katika ukurasa wangu. Nimeona leo niwahusishe na kuwaletea somo moja la “NAMNA YA KUTUMIA WHATSAPP KIBIASHARA”. Nyote ni mashaidi kuwa linapokuja suala la mitandao ya kijamii, WHATSAPP imetokea kuwa na matumizi makubwa kutokana na mfumo wa kutumia UJUMBE kutoka kwa mtu kwenda kwa mwingine (personalized messages). Hii inaufanya mtandao huu wa Kijamii kwa sasa kuwa maarufu katika Ulimwengu wa Digitali na unatumika kama kifaa cha kuendeleza biashara hasa suala la utafutaji wa MASOKO NA FURSA. Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2014 uko India, WhatsApp ilitumiwa kwa wingi na nguvu na Vyama vya Kisiasa kama chombo cha kuwafikia wapiga kura kwa urahisi. Matokeo yalikuwa makubwa,kwa Vyama Vya Siasa kupeleka Ujumbe wa kuelezea SERA zao kwa wananchi kwa haraka na muda mfupi. Nipende kusema siyo Wanasiasa tu wa India lakini hata hapa Nchini kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015,tumejionea jinsi habari za Uchaguzi na Kampeni kutoka kwa Wagombea zilivyo kuwa zinatufikia kwa urahisi kupitia WhatsApp. Mkakati huu wa kujitangaza kwa Wafanyabiashara, Watoa Huduma, unatumiwa sana na wataalamu wa masoko kijiditali ( Digital Marketing Experts) kwa kutumia umaarufu wa WHASAPP na kukigeuza kama chombo cha KIMKAKATI CHA KUTAFUTA MASOKO (effective social media marketing tool).
Nani Ujiunganishe naye?
Kwanza katika shuguli yako unayofanya uwe Mkulima wa Nyanya, Vitunguu,uwe Muuza Duka, Mfugaji, Fundi Ujenzi, Fundi wa Mbao,Msafirishaji,Mgahawa, Mwenye Salon, Kiwanda cha Juisi, au Mtoa Huduma ya Afya na Shule, Wakala wa Bima, Mama/Baba Ntilie, Muuza Genge, Baa, Nyumba ya Kulala Wageni na Hoteli, Mvuvi, Mrina Asali, Mtoa Huduma za Kifedha kama Vicoba, Saccos na Benki, NGO na Mwanasiasa ni lazima ujiunganishe na Wateja wako ulionao na unaowajua tayari. Muunganiko huo utasaidia kujenga maelewano zaidi na wateja wako. Kwa kuwa wateja awa tayari wametumia bidhaa au huduma yako, watakuwa wazi kukubali bidhaa au huduma mpya utakayoileta sokoni. Kutuma Ujumbe wa kupromoti kwa kila mtu halimradi unaweza kuleta matokeo hasi kwa bidhaa au huduma unayotangaza tofauti na kama utalenga kwa wale wateja ambao uliwai kuwahudumia.
Makundi ya WhatsApp ( WhatsApp Groups)
Zao kubwa la WhatsApp ni kuwa inaruhusu utumiaji wa kundi la watu kujiunga wakiwa na lengo maalum linalowafanya waungane katika mtandao.Hata, hivyo unapoanza kufikiria kutumia Makundi ya WhatsApp kama chombo cha kutafuta masoko kwa bidhaa zako linaweza kuwa siyo wazo zuri. Kwani wateja wako wanaweza kuwa na mwamko wa kupenda mazao/bidhaa yako lakini hawahitaji uwaunganishe na wawe wanawasiliana. Waweza kujikuta wateja wameamua kujiondoa kwenye kundi. Ni muhimu mawasiliano ya kibiashara basi yabaki ya kibinafsi kati yako na mteja.
Jinsi ya Kujitangaza bidhaa au huduma kutumia WhatsApp;
Hapa ndipo kuna mtihani mkubwa!
Ni namna gani hasa itabidi kutangaza bidhaa/huduma yako kutumia WhatsApp? Kwa kuanzia unaweza kubadili picha yako ya utambulisho (profile picture)na kuweka hile haswa ya bidhaa yako. Mfano kama ni muuza maziwa basi weka picha ya mtu akimkamua Ng`ombe. Wengine uwa wanaweka logo ya kampuni badala ya picha binafsi.
Ukiweka picha ya huduma na bidhaa unayotoa inajenga umakini wa mteja kufuatilia zaidi. Baada ya hapo unaweza kuanza na kutuma picha na video za bidhaa au huduma unayozalisha kwa wateja kibinafsi kwani tayari una namba za simu zao i! Jambo lingine ni muhimu kuhakikisha kuwa kila picha na Video unayotuma inaambatana na maelezo mafupi kumfanya mteja aelewe kwa ufasaha. Mara ngapi na muda gani kutuma Ujumbe kwa Mteja wako? Hii tena ni muhimu sana! Huhitaji wateja wako wajifiche kwa kuwatumia ujumbe wa kujitangaza wenye maneno ya kitaalamu sana kiasi hawaelewi nini umeandika. Ukifanya hivi kitakachofuata ni wateja kuzuia wasione meseji zako tena ( blocking ). Watumie ujumbe rahisi kuelewa mmoja au mbili kwa wiki inatosha. Mkizoeana kwa muda sasa na wateja wako unaweza kutuma zaidi kwani wataona ni jambo la kawaida. WhatsApp kwa sasa ndio habari ya mjini linapokuja suala la Dunia ya Kidijitali. Watumiaji wa mtandao huu wanaongezeka kila siku na wanatumia muda mwingi hapa kuliko mitandao mingine ya kijamii. Ni mtandao ambao unaunganisha watu kirahisi kwa kutumia mawasiliano ya ujumbe,picha, video na sauti. Ni rahisi kujenga mahusiano ya kibiashara na wateja wako ukitumia mTandao huu hivyo kama hujaanza kutumia tafadhali unahimizwa kuutumia na kufikisha bidhaa na huduma zako kwa wateja na kwa gharama nafuu. NAMNA YA KUTUMIA WHATSAPP KIBIASHARA